Daktari wa Yanga Dk Shecky Mngazija amesema kiungo Mapinduzi Balama yuko tayari kurejea dimbani na sasa ataanza mazoezi wakati wowote
Balama amekuwa nje ya uwanja kwa takribani miezi minne akiuguza majeraha ya kifundo cha mguu aliyopata mwishoni mwa msimu uliopita
Kiungo huyo aliyewatungua Simba goli la 'kideoni' msimu uliopita, mashabiki wanamsubiri kwa hamu wamuone katika kikosi cha kocha Cedrick Kaze

"Balama ataanza rasmi mazoezi ya pamoja na wenzake hivi karibuni. Vipimo vya majeraha yake vinaonyesha amepona kwa kiasi kikubwa na tayari alikuwa ameanza mazoezi mepesi peke yake, tunaamini pindi timu itakaporejea jijini Dar es Salaam ataanza mazoezi ya pamoja na timu,” alisema Mngazija
Yanga tayari imerejea jijini Dar es salaam wakitokea mkoani Mwanza ambako jana walilazimishwa suluhu ya bila kufungana dhidi ya Gwambina Fc
Timu imeingia kambini kujiandaa na mchezo dhidi ya Simba utakaopigwa Jumamosi, Novemba 07 kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa