Uongozi wa Yanga ulipiga hesabu kali kuuhamishia mkoani Arusha mchezo wa ligi kuu dhidi ya Dodoma Jiji ambao utapigwa Jumamosi
Yanga ndio mwenyeji wa mchezo huo, na ulipaswa kupigwa uwanja wa Benjamin Mkapa lakini uongozi ukatumia fursa iliyotolewa na Bodi ya Ligi kwa kila timu kuchagua uwanja mmoja kucheza mechi nje ya uwanja wao rasmi
Ukiangalia kwa umakini ratiba ya Yanga, utaelewa kwa nini uongozi ulichukua uamuzi wa kuupeleka mchezo huo Arusha
Baada ya mchezo dhidi ya Mwadui Fc uliopigwa Shinyanga juzi, Yanga ilipaswa kurudi jijini Dar es salaam kucheza na Dodoma Jiji Disemba 19 kisha kusafiri mkoani Mbeya kucheza na Ihefu Fc Disemba 26
Wakitoka Mbeya watasafiri tena kule Sumbawanga kuifuata Tanzania Prisons Disemba 31
Kwa kuhamishia mchezo dhidi ya Dodoma Jiji mkoani Arusha, ina maana wachezaji watazoea mazingira ya viwanja kwani wamecheza Shinyanga, wanakwenda kucheza Arusha, kisha Mbeya na baadae Rukwa
Kimbinu, kocha Cedric Kaze ataiandaa timu yake vyema zaidi kwani mechi hizo nne zinapigwa katika mazingira yanayofanana
Ni tofauti na vile timu ingerejea jijini Dar es salaam kucheza mechi moja tu na kisha kubadili tena maandalizi kwa ajili ya mechi zilizofuata mikoani
Hivyo pamoja na uongozi kuwapa fursa mashabiki wa Arusha kuishuhudia timu yao, mpango huo utawarahisishia ratiba na kuwa na maandalizi mazuri