Kocha Mkuu wa Yanga Cedric Kaze amesema wataingia kwa tahadhari katika mchezo wa ligi kuu unaofuata dhidi ya Dodoma Jiji hapo kesho lakini kwao pointi tatu ni muhimu
Kikosi cha Yanga kilitua Arusha jana jioni na leo wanatarajia kukamilisha maandalizi yao ya mwisho kuelekea mchezo huo ambao utapigwa uwanja wa Sheikh Amri Abeid
Yanga iliweka kambi ya siku tatu mkoani Singida, wakicheza mchezo wa kirafiki dhidi ya Singida United na kupata ushindi wa mabao 3-0
Kaze amesema ili kuweza kufikia malengo waliyojiwekea, wanahitaji kupambana kuhakikisha wanapata matokeo katika kila mchezo
Amesema ligi ina ushindani, wanapaswa kuwa makini na kutorudia makosa ambayo yanajitokeza katika mechi za nyuma, ikiwamo suala la kutumia vema nafasi wanazotengeneza na umakini katika safu ya ulinzi na ushambuliaji.
"Ligi ina ushindani mkubwa, hatutadharau timu yoyote tutakayokutana nayo, hivyo tunaenda kucheza na Dodoma ambao sio wabaya wana kikosi kizuri na wamejipanga kutafuta pointi tatu, hata sisi tunahitaji kupata pointi tatu ili kufikia malengo yetu," alisema Kaze