Pamoja na kuwa nje ya uwanja kwa takribani wiki tatu, kiungo mshambuliaji wa Yanga Saido Ntibazonkiza jana alicheza mchezo wa fainali michuano ya kombe la Mapinduzi dhidi ya Simba akikomelea penati ya mwisho iliyoihakikishia Yanga taji la pili la michuano hiyo wakishinda kwa mikwaju ya penati 4-3
Akizungumza baada ya mchezo huo, Ntibazonkiza alisema kuwa hakuwa amefanya mazoezi kwa takribani wiki tatu kutokana na majeraha lakini aliona ni muhimu kuwa sehemu ya kikosi ambacho kilihitaji kushinda
Aidha Ntibazonkiza amefichua kuwa wachezaji wenzake walimtaka ashiriki mchezo huo kwa kuwa waliamini ataisaidia timu
"Nashukuru nimepiga penati ya mwisho ambayo imetupa ubingwa, mchezo haukuwa mwepesi lakini kwa upande wetu ilikuwa muhimu sana kuweza kushinda"
"Leo sikuwa vizuri sana kwani nilichokionyesha ni asilimia 50% tu ya kile ninachoweza kufanya uwanjani. Sikufanya mazoezi kwa wiki tatu tangu nilipoumia lakini nashukuru leo nimeweza kucheza kwa dakika zote 90 na kuisaidia timu"
"Kocha (Kaze) anaamini uwezo wangu na hata wachezaji wenzangu ambao mimi huwa nawaita wanangu kwani karibu wote nimewazidi umri, waliniomba leo nishiriki mchezo huu pamoja na kuwa sikuwa na mazoezi kwa muda mrefu. Nawaahidi Wanayanga kuwa wasubiri mambo mazuri zaidi kutoka kwangu hasa baada ya kupona majeraha," alisema Saido ambaye kwa sasa wanamuita 'Antibiotic'
Tangu atue Yanga Ntibazonkiza amefunga mabao matano na kutoka pasi tatu za mabao katika mechi tatu za ligi na mchezo wa kirafiki