Vinara wa ligi kuu ya Vodacom Yanga, majira ya saa moja usiku wa leo Jumamosi, Februari 20, watashuka uwanja wa Benjamin Mkapa kuikabili Mtibwa Sugar katika mwendelezo wa mikiki mikiki ya ligi
Baada ya kulazimishwa sare katika michezo mitatu mfululizo iliyopita, huu ni mchezo ambao Wananchi hawatakuwa na 'simile' kwani wanazihitaji kwelikweli alama tatu
Wachezaji, benchi la ufundi, viongozi na mashabiki wote kauli yao ni moja, lazima Mtibwa Sugar 'apasuke' kwa Mkapa leo
Mazingira hayo yanaufanya mchezo huo kuwa mgumu kwani nao Mtibwa Sugar wataingia wakitamani kuendelea kuivurugia Yanga katika mbio za kuwania ubingwa
Kauli ya msemaji wa Mtibwa Sugar Thobias Kifaru, kuwa Yanga wasitarajie mteremko katika mchezo huo kwani hata wao wamejipanga kuondoka na alama zote tatu
Baada ya kukutana na uongozi, wachezaji wa Yanga wameahidi kuwa leo watapambana kwa jasho na damu kuhakikisha wanapata ushindi
Nahodha Lamine Moro juzi alitoa kauli ya kuwatuliza mashabiki, akiwataka wajitokeze kwa wingi uwanja wa Benjamin Mkapa jioni ya leo
Kwa kocha Cedric Kaze huu ni mchezo wa kusahihisha makosa aliyofanya katika mchezo uliopita dhidi ya Kagera Sugar
Kikosi alichoanza nacho katika mchezo huo hasa kwa kumuacha nje kiungo Mukoko Tonombe kilikosolewa na wengi, madhara yake yalionekana
Kaze leo anatarajiwa kuanza na kikosi imara ambacho kinaweza kumpa alama zote tatu kwani hata kwa upande wake, matokeo tofauti na ushindi yanaweza kumuongezea presha