Aliyekuwa Kocha Mkuu wa Yanga Cedric Kaze ameushukuru uongozi wa klabu hiyo kumpa nafasi ya kufundisha kikosi cha mabingwa hao wa kihistoria
Kaze amesema anajivunia mafanikio aliyopata katika siku 142 ambazo amedumu na Yanga akifanikiwa kutwaa ubingwa wa kombe la Mapinduzi na kuiacha Yanga ikiwa kileleni
"Wananchi nimefurahi katika hii miezi mitano tumekuwa pamoja, tumepata furaha na tukapata wakati mgumu lakini ndivyo mpira wa miguu ulivyo. Wengi wamekosa subira"
"Naenda kifua mbele kwani naamini kwa muda nimekaa na timu tumewapa furaha kwa kuwapatia kikombe cha kwanza katika miaka mitatu," aliandika Kaze kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii
Kaze ameiongoza Yanga kwenye michezo 18 katika ligi, ameshinda michezo 10, ametoka sare michezo saba na kufungwa mchezo mmoja
Pia aliiongoza mechi nne kule visiwani Zanzibar kwenye michuano ya kombe la Mapinduzi, Yanga ikifanikiwa kuibuka mabingwa