Nani arithi mikoba ya Kaze?

Shabiki NambaMoja By Shabiki NambaMoja
β€’
8 Mar 2021
Nani arithi mikoba ya Kaze?

Jana baada ya mchezo dhidi ya Polisi Tanzania ambao ulimalizika kwa matokeo ya sare ya bao 1-1, uongozi wa Yanga ulichukua maamuzi magumu ya kulivunja benchi lote la ufundi lililokuwa likiongozwa na kocha Cedric Kaze

Ni uamuzi uliofikiwa baada ya mfululizo wa matokeo yasiyoridhisha. Katika michezo sita iliyopita kwenye ligi, Yanga imeshinda mchezo mmoja, sare michezo minne na kufungwa mchezo mmoja

Kimahesabu bado ni mapema kuiondoa Yanga katika mbio za ubingwa kwani kuna michezo 11 imesalia kwa upande wao huku watani zao Simba wakisalia na michezo 15, minne kati ya hiyo ikiwa ya viporo. Lakini pia bado kuna mechi kati yao, mchezo ambao Yanga watahitaji ushindi tu

Muhimu kwa uongozi ni kuhakikisha hawafanyi makosa katika uchaguzi wa benchi la ufundi

Ni wazi kwa muda uliobakia kumaliza msimu, kuleta kocha mpya ambaye hajawahi kufanya kazi hapa Tanzania hakuwezi kuiletea tija Yanga kwani hatakuwa na zaidi ya miezi miwili

Ni kawaida kwa makocha wapya kuhitaji muda wa kujenga timu, kwa sasa Yanga haina muda huo ndio maana wanapaswa kumleta kocha ambaye tayari anafahamu mazingira na kazi iliyo mbele yake

Pia uongozi unaweza kuunda benchi la ufundi la muda ili kukamilisha msimu kisha kuleta kocha mpya mwishoni wa mwa msimu

Miongoni mwa majina ya makocha ambao wanaweza kuisaidia Yanga wakati huu,  wa kwanza ni kocha Charles Mkwasa ambaye kwa sasa anainoa klabu ya Ruvu Shooting

Huyu ni kocha ambaye sio mgeni Yanga, amekuwa mchezaji, kocha na kiongozi kwa vipindi tofauti

Msimu huu ameifanya Ruvu Shooting kuwa moja ya timu zinazocheza kandanda safi na kupata matokeo

Ukimsikia Masau Bwire anatamba kuwa Ruvu Shooting ndio klabu inayocheza kandanda safi nchini kama 'Barcelona' ni kwa sababu ya kazi ya Mkwasa

Namini Mkwasa na kocha Juma Mwambusi (kama amepona maradhi yaliyokuwa yakimsumbua), wanaweza kuunda benchi imara la ufundi ambalo linaweza kuivusha Yanga salama katika michezo iliyobaki

Wananchi wanafahamu umuhimu wa Mwambusi kwani tangu alipoondoka Yanga baada ya michuano ya kombe la Mapinduzi, ndio mambo yakamuharibikia Kaze

Kocha wa pili ni Mwinyi Zahera. Mcongomani huyu akirejeshwa Yanga safari hii anaweza kufanya maajabu

Aliondolewa msimu wa 19/20 katika mazingira ya kutatanisha akipoteza mchezo mmoja tu kwenye ligi, viongozi wakitumia kigezo cha kutolewa michuano ya Kimataifa bila ya kujali mpinzani ambaye Yanga ilikutana nae

Zahera aliisimamia Yanga katika kipindi kigumu. Lakini timu iliweza kufanya vizuri. Huyu ni kocha mwenye mapenzi makubwa na Yanga, ni Mwananchi hasahasa, upendo wa mashabiki ulimfanya ajihisi Yanga ni nyumbani kwake

Kwa muda uliobaki, Yanga inahitaji kocha wa kuipa timu matokeo bila ya kujali kandanda wanalocheza. Kwani ukicheza kandanda la kuvutia bila ya kupata matokeo ni kazi bure

Zahera anaiweza kazi hiyo, tayari amedhihirisha na zaidi 'Papaa' ni zaidi ya kocha. Ni Mzazi, Mlezi na Mhamasishaji. Ndiye kocha ambaye anaweza kurudisha morali ya wachezaji juu na wakafanya vizuri

Kimbinu Zahera yuko vizuri, ni bahati mbaya wakati anaifundisha Yanga hakuwa na wachezaji aliowahitaji na hata usajili aliofanya haukuwa wa wachezaji bora sana kwani alipewa bajeti ndogo ya usajili

Lakini wapo wachezaji ambaye yeye aliwasajili kwa 'bei chee' mfano David Molinga, Patrick Sibomana wangekuwa katika kikosi cha msimu huu pengine wangefanya vizuri

Kocha wa tatu ni Hans Van Pluijm. Iko hoja kuwa babu Hans mwenye umri wa miaka 72, kwa sasa anaweza asimudu mikiki mikiki ya ligi

Lakini Van Pluijm ndiye kocha wa mwisho kuwapa mashabiki wa Yanga furaha ya kweli. Ni kocha wa mwisho kuwafanya watu watambe na kutembea kifua mbele. Wakati wake Yanga ilicheza vizuri na kupata matokeo katika mechi zake

Ng'ombe hazeeki maini, umri unaweza kuwa umemtupa mkono lakini bado elimu yake ya ukocha anayo

Pluijm, Mkwasa na Mwambusi hawa ni makocha waliofanya kazi pamoja wakati ule na hata sasa wanaweza kufanya kazi pamoja kuivusha katika kipidndi hiki

Yapo majina ya makocha ambao wanatajwa kama Etienne Ndayiragije na Meckie Mexime lakini kwa maoni yangu, hawawezi kuleta maajabu Yanga

Kwa sasa Yanga inahitaji kocha ambaye akifika tu kambini mambo yabadilike sio kocha wa kuhitaji mwezi mmoja kujenga kikosi kwani huo muda sasa haupo

ADVERTISE HERE

Yanga SC Stories

Magoli; Yanga 2-1 Mashujaa Fc, NBC PL (FT)
Magoli; Yanga 2-1 Mashujaa Fc, NBC PL (FT)
5h ago
READ MORE β†’
FT : Yanga 2-1 Mashujaa Fc, NBC PL, Oct 27
FT : Yanga 2-1 Mashujaa Fc, NBC PL, Oct 27
5h ago
READ MORE β†’
Kikosi : Yanga vs Mashujaa Fc, NBC PL, Oct 27
Kikosi : Yanga vs Mashujaa Fc, NBC PL, Oct 27
8h ago
READ MORE β†’
Yao bado kidogo, Diarra tayari kurejea
Yao bado kidogo, Diarra tayari kurejea
13h ago
READ MORE β†’
Matchday; Yanga vs Mashujaa Fc, NBC PL, Oct 27
Matchday; Yanga vs Mashujaa Fc, NBC PL, Oct 27
16h ago
READ MORE β†’
Yanga inahitaji utulivu, si vita ya lawama
Yanga inahitaji utulivu, si vita ya lawama
17h ago
READ MORE β†’
Magazeti ya leo Jumanne, Oktoba 27 2026
Magazeti ya leo Jumanne, Oktoba 27 2026
19h ago
READ MORE β†’
Maandalizi ya kuikabili Mashujaa Fc yamekamilika
Maandalizi ya kuikabili Mashujaa Fc yamekamilika
1d ago
READ MORE β†’
Aziz Ki amemaliza adhabu, tayari kurejea kikosini
Aziz Ki amemaliza adhabu, tayari kurejea kikosini
1d ago
READ MORE β†’
Tunajua tumewaumiza, tuko tayari kupambana - Dladla
Tunajua tumewaumiza, tuko tayari kupambana - Dladla
1d ago
READ MORE β†’