Simba kumalizana na Sawadogo

Joel JJ By Joel JJ β€’ 30th June 2023


Simba kumalizana na Sawadogo

Uongozi wa Simba umesema wanatumia utaratibu mzuri kulingana na vipengele vya mikataba yao na wachezaji inapofika hatua ya kuachana na mchezaji ambaye bado mkataba wake na klabu upo hai, jambo ambalo pia wanalitekeleza kwa kiungo mkabaji Ismael Sawadogo

Kauli hiyo imetolewa na Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba, Ahmed Ally, baada ya madai kuwa klabu hiyo inashindwa kuachana na Sawadogo kutokana na kuitaka kumlipa Sh. milioni 700 ili kuvunja mkataba wake.

Ahmed amesema mchezaji anaposaini mkataba na Simba kuna makubaliano yanakuwapo mwanzoni ya jinsi ambavyo akishindwa kuendelea kuitumikia klabu hiyo au viongozi wakihitaji kuvunja mkataba wanachotakiwa kukifanya kwanza.

Alisema Sawadogo ana mkataba wa mwaka mmoja na wako kwenye mazungumzo ya kutoendelea naye kwa msimu ujao na baada ya maafikiano ya pande zote mbili wataweka wazi kuachana naye rasmi.

Ahmed alisema Simba inaendeshwa kisasa katika mazungumzo hayo na si suala la fedha kwa sababu kabla ya kusaini mkataba kuna kipengele ambacho kiko wazi mchezaji au klabu atakapovunja mkataba na anapouzwa nini kifanyike kabla.

"Hayo masuala la Sh. milioni 700 sijui yametoka wapi kwa sababu kila kitu kipo wazi, ni kweli Sawadogo hatutaendelea naye kwa msimu ujao na tuko kwenye mazungumzo ya kuvunja mkataba wake," alisema Ahmed

Aliongeza kuwa suala la fedha ya kumlipa mchezaji halijadiliwi bali linakuwapo kwenye mkataba ambao wanaingia naye anaposaini kuitumikia klabu hiyo na hadi sasa hakuna mchezaji ambaye ameachana nao anayedai haki zake.


  

XTRA 90 INSIDER

Get the latest tactics & rumors delivered to your inbox.