Simba kusaka rekodi nyingine Angola leo

Joel JJ By Joel JJ β€’ 12th January 2025


Simba kusaka rekodi nyingine Angola leo

Simba Sc leo usiku itashuka kwenye Uwanja wa Novemba 11, Luanda, Angola kumenyana na Bravos katika mchezo wa raundi ya tano hatua ya makundi kombe la Shirikisho (CAF CC)

Matarajio ya mashabiki wa Simba leo ni kuona timu yao inafanya kile ilichokifanya miaka 31 iliyopita ilipofanikiwa kufuzu hatua ya fainali ya Kombe la CAF, ambalo sasa linaitwa Kombe la Shirikisho, dhidi ya Atletico Spotivo Aviacao, ikiwa ugenini

Leo Simba inahitaji ushindi au sare ili kufuzu hatua ya robo fainali kutoka Kundi A. Kama itafanikiwa kufanya hivyo, itakuwa ni mara ya pili kwani mwaka 1993, Simba ilifanikiwa kuingia hatua ya fainali ya Kombe la CAF, ilipotoka suluhu dhidi ya Atletico Spotivo Aviacao ikiwa nchini humo, katika mchezo wa marudiano baada ya mchezo wa kwanza uliochezwa Uwanja wa Taifa Dar es Salaam (sasa Uhuru), Simba kupata ushindi wa mabao 3-1

Iwapo itapata ushindi pia itakuwa ni mara ya pili kwani ikiwa nchini humo, Oktoba 9 mwaka 2022, iliichapa Primeiro de Agosto mabao 3-1, katika mchezo wa raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa huku wa marudiano uliochezwa nchini, Oktoba 16, 2022, Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, ilishinda bao 1-0, na kufanikiwa kutinga hatua ya makundi

Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids, amesema maandalizi yote ya mchezo huo yamekamilika huku akisema atakwenda kuikabili Bravos do Maquis kwa mfumo tofauti. Alisema kuwa timu hiyo ni hatari inapokuwa nyumbani, ikipenda zaidi kumiliki mpira, hivyo ametengeneza mkakati wa kuhakikisha wanawanyima fursa hiyo

Bravos wameshinda mechi zote walizocheza nyumbani katika kombe la Shirikisho msimu huu hivyo ni wazi vijana wa kocha Fadlu Davids watahitaji kuwa katika ubora wao kuhakikisha hawapotezi mchezo huo


  

XTRA 90 INSIDER

Get the latest tactics & rumors delivered to your inbox.