Uongozi wa Yanga umeweka mkakati wa kuhakikisha msimu ujao wanarejea kwa nguvu kubwa katika michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika
Baada ya kucheza fainali ya kombe la Shirikisho 2022/23 na pia kucheza robo fainali ya ligi ya mabingwa 2023/24, msimu huu Wananchi hawakufanikiwa kuvuka hatua ya makundi
Ikiongoza ligi kuu ya NBC ikiwa na alama 70, Yanga tayari imejihakikishia tiketi ya kucheza ligi ya mabingwa msimu ujao
Katika moja ya mahojiano yake, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga Ali Kamwe amesikika akitamba kuwa tayari wameanza mchakato wa maboresho ya kikosi ili kuhakikisha msimu ujao wanakuwa bora zaidi hasa katika michuano ya Kimataifa
"Sisi tayari tumejihakikishia tiketi ya kucheza ligi ya mabingwa msimu ujao, Niwaambie tu Wanachama na mashabiki wa Yanga, msimu ujao hatutaki yaliyotokea msimu huu yajirudie"
"Tunataka kufanya vizuri zaidi katika michuano ya ligi ya mabingwa hivyo tutarajie maboresho makubwa ya kikosi chetu," alisema Kamwe
Taarifa za ndani zimedokeza kuwa huenda Yanga ikaongeza wachezaji 6 katika dirisha kubwa litakalofunguliwa mwezi Julai
Maeneo ambayo yanatarajiwa kuwa na maboresho ni safu ya ulinzi hasa mlinzi wa kushoto, kati, kiungo mkabaji, kiungo mshambuliaji na mshambuliaji wa kati
Majina yanayotajwa kuwa kwenye rada ya Yanga ni pamoja na Jonathan Sowah, Feisal Salum, Koimizo Maiga (kiungo mkabaji kutoka Asec) na Agee Basiala Amongo (kiungo mshambuliaji As Maniema Union)
Lakini pia wamo beki Hennock Inonga Baka(FAR Rabat) na kiungo mshambuliaji Arthur Bada kutoka Singida BS ambaye alibadili uraia wake wa Ivory Coast na kuwa Mtanzania



