Wazee wa klabu ya Yanga wametishia kwenda Mahakamani kuzuia kutangazwa bingwa wa ligi kuu msimu huu kama Yanga haitatendewa haki huku wakiitaka TPLB kutoka hadharani kutaja sababu iliyopelekea kuahirisha mchezo namba 184 kati ya Yanga dhidi ya Simba uliopaswa kupigwa March 08 katika uwanja wa Benjamin Mkapa
Akizungumza baada ya kuhitimishwa kwa Mkutano uliowakutanisha wazee wa Yanga uliofanyika Makao Makuu ya klabu, Jangwani, Mzee Msumi amesema watakwenda Mahakamani kuzuia bingwa wa ligi kuu msimu kutangazwa mpaka pale ufafanuzi wa kisheria utakapotolewa na TPLB/TFF
"Hatuwezi kuwaacha watu wachache wanaotaka kuleta vurugu kwa kisingizio kutumia klabu yetu, sisi tutakwenda Mahakamani tukazuie asitangazwe bingwa mpaka ufafanuzi wa kisheria utoke au waje Mahakamani watuthibitishie flani na flani wametoa rushwa au wamefanya hivi"
"Ifahamike kuna watu wametumia gharama kubwa, wametoka mikoani, wametoka nje ya nchi wamekata tiketi ili kushuhudia dabi, sisi tumeamua kuwatetea ili kulinda heshima ya mpira wa Tanzania"
"Hatutajali eti kuna mashindano ya Afcon, kwa sababu hii ni haki yetu ya msingi na tunataka tupate ufafanuzi wa tuhuma zilizotolewa," alisema Mzee Msumi
Wazee wa Yanga wamesisitiza kuwa klabu hiyo sio ya Injinia Hersi Said au Makamu wake Arafat Haji bali ni ya Wanachama wa Yanga
Hivyo wanaunga mkono msimamo wa klabu kutocheza mechi iliyotangazwa na Bodi ya ligi Juni 15 kwa sababu hakuna maelezo yaliyotolewa juu ya kanuni iliyotumika kuahirisha mechi hiyo namba 184
Lakini pia wazee wamesema hawajapata maelezo ya hatua zilizochukuliwa dhidi ya wale waliotuhumiwa kusababisha mchezo huo kutochezwa
"Moja ya matamko yao (klabu ya Simba), walitangaza wao hawatacheza mechi yoyote mpaka wale waliohusika kuwazuia kufanya mazoezi wachukuliwe hatua, lakini hakuna chochote kilichofanyika zaidi ya kutangazwa tarehe nyingine"
"Hatujui nani aliahirisha mechi, hatujui kanuni gani ilitumika kuahirisha mechi na hatujui ni hatua gani wale waliohusika wamechukuliwa"



