Mashabiki wa soka nchini Tanzania na hasa visiwani Zanzibar wanatarajiwa kushuhudia mtanange wa kusisimua wa fainali ya Kombe la CRDB kati ya mabingwa watetezi Yanga SC dhidi ya Singida Black Stars. Mchezo huu wa kuamua bingwa wa msimu huu umepangwa kuchezwa tarehe 28 Juni katika dimba la kisasa la New Amaan Complex, Zanzibar.
Hii ni mara ya pili mfululizo kwa fainali hiyo kupigwa katika uwanja wa New Amaan Complex, jambo linaloendeleza mvuto wa soka visiwani humo na kuonyesha namna Zanzibar inavyozidi kuwa kitovu muhimu cha matukio makubwa ya michezo nchini.
Katika msimu uliopita, Yanga walinyakua taji hilo katika uwanja huo huo wa Amaan baada ya ushindi wa mikwaju ya penati 6-5 dhidi ya Azam FC, kufuatia sare tasa ya bila kufungana katika muda wa kawaida na nyongeza. Huu ulikuwa ushindi wa tatu mfululizo kwa Yanga, ambao sasa wanalisaka taji hili kwa msimu wa nne mfululizo
Awali, fainali ya mwaka jana ilipangwa kuchezwa katika uwanja wa Tanzanite Kwaraa ulioko Manyara, lakini kutokana na uwanja huo kutokuwa tayari, mchezo huo ukahamishiwa rasmi Zanzibar
Singida Black Stars, walitinga fainali kwa mara ya kwanza wakiiondosha Simba kwa ushindi wa mabao 3-1 katika mchezo wa nusu fainali huku Yanga ikitangulia fainali kwa ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya JKT Tanzania
Bila shaka itakuwa fainali ya aina yake, mara ya mwisho Yanga na Singida BS zilikutana Zanzar katika mechi ya ligi kuu, Yanga ikiibuka na ushindi wa bao 1-0 katika mechi ambayo ilikuwa na mchuano mkali



