Klabu ya Azam FC imeanza rasmi harakati za kuhakikisha haitingishwi na uwezekano wa kuondokewa na Feisal Salum 'Fei Toto', kiungo wake tegemezi ambaye kwa sasa yupo katika rada za klabu kubwa kama Simba, Yanga, na Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini.
Ingawa Azam haijaweka wazi hatma ya kiungo huyo, tafsiri ya kiufundi ni wazi klabu hiyo ipo kwenye maandalizi ya mapema kufidia nafasi ya Fei Toto endapo ataondoka msimu ujao.
Azam tayari wamesisitiza kuwa mchezaji huyo hatauziwa chini ya Sh1 bilioni, licha ya kuwa bado na mkataba wa mwaka mmoja.
Katika mchakato huo, Allan Okello, kiungo mshambuliaji wa Vipers mwenye uwezo mkubwa wa kutumia mguu wa kushoto, ndiye anayeonekana kuwa chaguo la kwanza.
Okello si jina geni katika soko la usajili Afrika Mashariki; klabu ya Simba pia iliwahi kumuwinda katika dirisha dogo la usajili lililofunguliwa Desemba 15 mwaka jana, lakini iligonga mwamba kutokana na msimamo mkali wa Rais wa Vipers, Lawrence Mulindwa, ambaye huwa hana urahisi wa kuuza nyota wake muhimu.
Kwa msimu huu pekee, Okello ameonyesha kiwango cha juu akifunga mabao 19, akiwa katika msimu wake wa pili tangu arudi Vipers.
Klabu hiyo pia inaongoza Ligi Kuu ya Uganda baada ya mechi 30, ikiwa imeshinda 21, sare 6 na kupoteza 3 rekodi inayoonyesha mchango mkubwa wa Okello.



