Kikosi cha Yanga tayari kimewasili Malawi kuelekea mchezo wake wa mkondo wa kwanza kuwania tiketi ya kutinga hatua ya makundi ya michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika (CAFCL) dhidi ya Silver Strikers
Ujio wa kocha msaidizi Patrick Mabedi raia wa Malawi unatajwa kuirahisishia kazi Yanga kuelekea kuwakabili Silver Strikers kwani anaifahamu vyema timu hiyo
Hii ni habari njema kwa kocha Romain Folz ambaye ujio wa Mabedi umefanya kazi ya maandalizi ya timu kuelekea mchezo huo kuwa nyepesi
Folz amesema alikuwa na taarifa kidogo kuhusu klabu ya Silver Strikers lakini ujio wa Mabedi, amepata taarifa zaidi
Kocha huyo raia wa Ufaransa amefichua kuwa Silver Strikers wana ubora katika eneo lao la kiungo hivyo wanapaswa kuandaa mpango mkakati wa kuwadhibiti
"Nimepewa taarifa Silver Strikers ni timu inayoundwa na wachezaji vijana na wanacheza kwa nidhamu sana, lakini ubora wao mkubwa upo kwenye eneo la kiungo"
"Kuwadhibiti lazima tutengeneze mpango wa kuvunja ubora wa safu yao ya kiungo, Yanga ina safu nzuri ya ushambuliaji ambayo imejipanga kuhakikisha inaulazimisha ukuta wa ulinzi kufanya makosa," alisema
Mabedi amecheza ngazi ya klabu na hata kufundisha timu ya Taifa ya Malawi akikamilisha majukumu yake mwaka huu kabla ya kutua Yanga



