CAFCC: Hatma ya Azam Fc mikononi mwa Maniema Union

Joel JJ By Joel JJ β€’ 7th February 2026


CAFCC: Hatma ya Azam Fc mikononi mwa Maniema Union

Azam FC leo Jumamosi, Februari 7, 2026, itashuka dimbani kuivaa Maniema Union ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) katika mchezo wa raundi ya tano ya hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika (CAF Confederation Cup). Pambano hilo litapigwa kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.

Mchezo huo ni wa Kundi B na unatajwa kuwa wa maamuzi kwa Azam katika harakati zao za kusaka tiketi ya kufuzu hatua ya robo fainali ya michuano hiyo.

Kwa mujibu wa msimamo wa kundi hilo kabla ya mchezo wa leo, Wydad wanaongoza wakiwa na alama tisa sawa na Maniema Union baada ya michezo minne, huku Azam FC wakishika nafasi ya tatu wakiwa na alama sita. Ushindani wa kundi hilo bado uko wazi, jambo linalofanya matokeo ya leo kuwa na uzito mkubwa katika kuamua hatma ya timu zitakazovuka hatua ya makundi.

Katika mchezo wa kwanza kati ya timu hizo uliochezwa ugenini, Azam walipoteza kwa mabao 2-0, matokeo yanayoongeza presha kwa wawakilishi hao wa Tanzania kutafuta ushindi nyumbani ili kufufua matumaini yao ya kufuzu.

Azam wanahitaji ushindi ili kufikisha alama tisa na kusogea karibu na kilele cha kundi, huku wakisubiri matokeo ya mchezo mwingine wa kundi hilo. Sare au kipigo vitaweka mazingira magumu zaidi kwa timu hiyo kuelekea raundi ya mwisho.

Kwa upande wa Maniema Union, ushindi leo utawapa alama 12 na kuwaweka katika nafasi nzuri ya kutinga robo fainali mapema. Hata sare inaweza kuwa matokeo chanya kwao.

Wawakilishi wengine wa Tanzania katika michuano hiyo Singida Black Stars watashuka dimbani kesho Jumapili kuikabili CR Belouizdad katika uwanja wa New Amaan Complex.


  

XTRA 90 INSIDER

Get the latest tactics & rumors delivered to your inbox.