Mshambuliaji wa Yanga Clement Mzize amekamilisha matibabu yake nchini Afrika Kusini akitarajiwa kuwa nje ya uwanja kwa takribani miezi minne.
Baada ya kuandamwa na mfululizo wa majeraha, uongozi wa Yanga umechukua hatua ya kuhakikisha nyota huyo anapata matibabu sahihi na kupata muda mrefu wa kuponya jeraha lake kabla ya kurudi tena uwanjani.
Mzize aliumia mwanzoni mwa msimu Septemba 27, 2025, katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Wiliete Benguela ya Angola na kuanza mchakato mrefu wa matibabu pamoja na upasuaji wa Desemba 2025, kabla ya kurudi tena kikosini.
Baada ya kurejea mshindi huyo wa tuzo ya Bao Bora la Mwaka 2025 ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), alijitonesha wakati wa maandalizi ya mechi ya mwisho ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya dhidi ya JS Kabylie.
Kwa mujibu wa daktari wa klabu ya Yanga, Moses Etutu, Mzize atakuwa nje ya uwanja hadi kufikia mwisho wa msimu huu na hivyo kutarajiwa kurudi kucheza tena katika msimu ujao wa mashindano



