Simba imetakata uwanja wa Airtel huko Singida ikiibuka ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Singida BS katika mchezo wa ligi kuu ya NBC.
Ulikuwa mchezo mgumu lakini Simba imetumia uzoefu wake kuchomoza na ushindi huo muhimu ugenini.
Mapema tu dakika ya 7 Anicet Oura alifungua akaunti yake ya mabao kwenye ligi akiifungia Simba bao muhimu baada ya walinzi wa Singida BS kuzembea kuondoa hatari langoni kwao.
Hata hivyo Singida BS walirejea mchezoni dakika chache kabla ya mapumziko Mossi akifunga bao la kichwa akimalizia krosi ya Lamine Jarjou.
Kipindi cha pili ni Singida iliyokuwa ikionekana hatari kupitia mashambulizi ya kushitukiza na katka matukio mawili wachezaji wao Khalid Aucho na Joseph Guede walionekana kama kufanyiwa madhambi ndani ya eneo la hatari lakini matukio hayo hayakumshawishi mwamuzi wa mchezo huo kutoa mkwaju wa penati.
Alikuwa 'super sub' Elie Mpanzu aliyepeleka kilio Singida BS akifunga bao la ushindi dakika ya 85 akimalizia krosi ya Clatous Chama baada ya kuwazidi mbio walinzi wa Singida BS waliokuwa wakidhani ameotea.

Ni alama tatu muhimu kwa Simba ambazo zinawafanya wasogee kwenye nafasi ya tatu katika msimamo wakifikisha alama 27.
Mapema TRA United iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Namungo Fc katika mchezo uliopigwa uwanja wa Black Rhino, Manyara.



