Klabu ya Tanzania Prisons, imeanza kuandika upya simulizi yao kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya kupata mfululizo wa matokeo chanya yaliyoibua matumaini mapya ya kusalia kwenye ligi hiyo msimu huu.
Baada ya mwanzo mbaya ulioifanya timu hiyo kupitia kipindi kigumu kilichoshuhudia uongozi ukifanya mabadiliko ya benchi la ufundi, sasa mwanga unaanza kuonekana ndani ya kikosi hicho cha Jeshi la Magereza. Ushindi wa mechi tatu mfululizo umebadilisha kabisa hali ya hewa kambini na kurejesha imani kwa mashabiki.
Katika michezo yao ya karibuni, Tanzania Prisons imeonyesha uimara mpya. Kwanza waliibuka na ushindi wa mabao 3-2 ugenini Mwanza, kisha wakarejea Uwanja wa Sokoine na kuifunga Dodoma Jiji mabao 3-1, kabla ya kumalizia mfululizo huo kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya JKT Tanzania.
Matokeo hayo yameiwezesha Prisons kupanda hadi nafasi ya 14 kwenye msimamo wa ligi wakiwa na pointi 26, hatua inayowapa nafasi ya kupigania kubaki salama msimu huu badala ya kuangukia kwenye presha ya kucheza mechi za mchujo.
Kwa sasa, kikosi hicho kina mechi tatu muhimu zilizobaki ambazo zinaweza kuamua kabisa hatma yao ya ligi. Wanatarajiwa kuanza dhidi ya Singida Black Stars Juni 24 mjini Singida, kabla ya kurejea Mbeya kumenyana na Mtibwa Sugar, na baadaye kumalizia ugenini dhidi ya Mashujaa FC.
Mchezo dhidi ya Singida Black Stars unaonekana kuwa wa βmaamuzi mapema,β ukizingatiwa ushindani wa alama ulivyo karibu katika sehemu ya chini ya msimamo.
Nahodha wa Tanzania Prisons, Lambart Sabiyanka, amekiri wazi kuwa hali ya timu sasa ni tofauti na ilivyokuwa mwanzo wa msimu. Kwa mujibu wake, ushindi huo umeongeza morali na umoja ndani ya kikosi.
Amesema mchezo dhidi ya Singida Black Stars una nafasi kubwa ya kuamua mwelekeo wa Prisons kwenye msimu huu, akisisitiza kuwa lengo lao ni kuepuka kabisa mashindano ya mchujo wa kushuka daraja.
βSingida Black Stars wameshikilia pakubwa hatma yetu. Tukivuka salama tunaweza kupata nafuu kubwa,β amesema Sabiyanka.
Ameongeza kuwa kila mchezaji sasa anapigania nembo ya klabu hiyo kwa bidii kubwa, huku akisisitiza umuhimu wa kucheza kwa tahadhari na hesabu sahihi katika mechi zilizobaki.



