Licha ya matokeo yasiyoridhisha ya timu ya taifa ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DR Congo) kwenye Kombe la Dunia 2026, shabiki maarufu Michel Kuka Mboladinga, anayefahamika zaidi kwa jina la "Lumumba Vea", ameendelea kuwa moja ya vivutio vikubwa vya mashindano hayo.
Lumumba Vea amevutia macho ya mashabiki na vyombo vya habari duniani kutokana na namna yake ya kipekee ya kuishangilia timu ya taifa ya DR Congo. Tofauti na mashabiki wengine wanaoshangilia kwa kelele na nyimbo, yeye husimama bila kutikisika kwa dakika zote 90 za mchezo akiwa ameinua mkono mmoja juu, akiiga sanamu la shujaa wa uhuru wa Congo, Patrice Lumumba, lililopo mjini Kinshasa.
Umaarufu wake ulianza wakati wa AFCON 2025, lakini safari hii ya Kombe la Dunia imemfanya kujulikana zaidi kimataifa. Hata baada ya DR Congo kushindwa kufurukuta uwanjani, kamera za televisheni zimeendelea kumfuatilia Lumumba Vea mara kwa mara, huku picha na video zake zikisambaa kwa kasi kwenye mitandao ya kijamii.
DR Congo ilianza kampeni yake kwa sare ya mabao 1-1 dhidi ya Ureno kabla ya kupoteza mchezo wa pili kwa bao 1-0 dhidi ya Colombia, hali iliyoiweka katika wakati mgumu wa kusaka nafasi ya kutinga hatua ya mtoano. Hata hivyo, ari ya Lumumba Vea haijapungua, akiendelea kuwa alama ya uzalendo na matumaini kwa mashabiki wa taifa hilo.
Katika moja ya mahojiano yake, Lumumba Vea alizungumzia namna yake y kusimama bila kutikisika si burudani bali ni heshima kwa historia ya taifa lake na kumbukumbu ya Patrice Lumumba, mmoja wa viongozi muhimu katika harakati za uhuru wa DR Congo.






