Vyanzo vya kuaminika vinaeleza kuwa klabu ya Yanga SC imeanza mazungumzo ya awali na aliyekuwa kocha wa Raja Casablanca, Fadlu Davids, kuhusu uwezekano wa kuchukua nafasi ya ukocha mkuu wa mabingwa hao wa kihistoria.
Taarifa hizo zinaeleza kuwa uongozi wa Yanga umemvutia sana kocha huyo raia wa Afrika Kusini kutokana na rekodi yake ya mafanikio katika klabu mbalimbali barani Afrika, ikiwemo kuiboresha Simba SC na kuifikisha fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika (CAF Confederation Cup).
Fadlu aliondoka Raja Casablanca hivi karibuni kwa makubaliano ya pande zote mbili baada ya timu hiyo kupoteza michezo miwili mfululizo katika Ligi Kuu ya Morocco na kupoteza matumaini ya kutwaa ubingwa.
Inaelezwa pia kuwa Yanga imekuwa ikimfuatilia kocha huyo kwa muda, hasa kutokana na uwezo wake wa kujenga timu zenye nidhamu ya kiufundi na uwezo wa kushindana kimataifa, jambo lililoonekana wazi alipokuwa Simba SC ambapo aliwafanya Wekundu hao wa Msimbazi kufanya vizuri kwenye mashindano ya CAF.
Kwa sasa, taarifa zinaeleza kuwa mazungumzo bado yako katika hatua za awali, huku pande zote mbili zikijadiliana masharti kabla ya kufikia makubaliano yoyote rasmi. Hata hivyo, dalili zinaonyesha kuwa kocha huyo yuko tayari kujiunga na Yanga endapo makubaliano yatakamilika.
Kwa sasa Yanga inanolewa na kocha Abdihamid Moalin baada ya kuachana na Pedro Goncalves raia wa Ureno



