Mmiliki wa Azam FC, Jamal Bakhresa, ameripotiwa kueleza kutoridhishwa kwake na namna mamlaka za soka nchini zinavyoendesha baadhi ya masuala yanayohusu klabu yake, akidai kuwa kuna hali ambayo inaifanya Azam FC kuhisi kutotendewa haki.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Bakhresa amesema endapo Azam FC itaendelea kuona haithaminiwi ndani ya mfumo wa soka la Tanzania, klabu hiyo inaweza kufikiria kujiondoa kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara na kushiriki Ligi Kuu ya Zanzibar.
Aidha, akizungumzia tukio la ugawaji wa medali, Bakhresa amedai kuwa medali iliyotolewa kwa Mtendaji Mkuu (CEO) wa Azam FC ilikuwa ni ya kiongozi huyo binafsi na si ya timu nzima, akisisitiza kuwa ikiwa ndivyo ilivyo, basi mhusika anapaswa kuihifadhi yeye mwenyewe.
Hata hivyo, Bakhresa ametoa wito kwa viongozi wa mpira wa miguu nchini kufanya maamuzi yenye kuzingatia haki, uwazi na maslahi mapana ya maendeleo ya soka la Tanzania, akisisitiza kuwa ustawi wa mchezo huo unapaswa kuwa kipaumbele kwa wadau wote.



