Tasnia ya soka imepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha aliyekuwa kipa wa Yanga SC, Clause Kindoki, ambaye amefariki dunia jana, Julai 11, 2026, kufuatia ajali mbaya ya bodaboda iliyotokea nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DR Congo).
Kwa mujibu wa aliyekuwa meneja wa mshambuliaji Fiston Mayele, Nestor Mutuale, Kindoki alipata ajali hiyo saa chache baada ya kumalizika kwa mchezo ambao timu yake ya Bustras iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Et Dauphin. Inaelezwa kuwa baada ya mechi hakusafiri na basi la timu, bali aliamua kutumia bodaboda, ndipo akahusika katika ajali iliyohusisha lori la mizigo.
Kindoki aliwahi kuitumikia Yanga SC katika msimu wa 2018/19 chini ya kocha Mwinyi Zahera, ambapo alisajiliwa pamoja na mshambuliaji Heritier Makambo. Ingawa alidumu kwa kipindi kifupi ndani ya kikosi hicho, alibaki kuwa sehemu ya historia ya klabu hiyo.
Baada ya kustaafu kucheza soka, Kindoki aliendelea kulitumikia mchezo huo akiwa kocha wa makipa wa Bustras, akijikita katika kuibua na kuendeleza vipaji vya makipa vijana nchini DR Congo.
Kifo chake kimeacha simanzi kubwa kwa familia, marafiki, wachezaji wenzake wa zamani na wadau wa soka wa Tanzania na DR Congo, wengi wakimkumbuka kwa kujituma kwake ndani na nje ya uwanja. Xtra90 inatoa salamu za pole kwa familia ya marehemu, ndugu, jamaa, marafiki na wote walioguswa na msiba huu mzito. Pumzika kwa amani, Clause Kindoki.