Klabu ya Singida Black Stars imeendelea kuimarisha safu yake ya ushambuliaji baada ya kukamilisha usajili wa mshambuliaji chipukizi Candidat Mapendo kutoka AS Dauphin Noir ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DR Congo).
Mapendo, mwenye umri wa miaka 19, amekuwa mmoja wa washambuliaji wanaozungumziwa zaidi katika soka la Congo baada ya kufanya vizuri katika Ligi Kuu ya DR Congo (Linafoot), ambako aliibuka kinara wa mabao kwa kufunga jumla ya mabao 22.
Mshambuliaji huyo aliiongoza AS Dauphin Noir kwa kiwango bora msimu uliopita, akiwa mhimili mkubwa katika safu ya ushambuliaji ya timu hiyo. Uwezo wake wa kufunga mabao muhimu katika nyakati tofauti ulimfanya kuwa mchezaji wa kuangaliwa kwa karibu na vilabu mbalimbali ndani na nje ya Congo.
Kutokana na kiwango chake, baadhi ya vyombo vya habari nchini Congo vimemtaja Mapendo kama mmoja wa washambuliaji chipukizi wenye matumaini makubwa katika kizazi kipya cha soka la taifa hilo.
Mbali na kutwaa tuzo ya ufungaji bora, Mapendo ameandika historia kwa kuweka takwimu zinazovutia akiwa bado na umri mdogo. Kasi yake ya kufumania nyavu imemfanya kulinganishwa na baadhi ya majina makubwa yaliyowahi kung’ara katika soka la Congo, akiwemo Trésor Mputu.