Aliyekuwa kiungo mahiri wa Yanga SC, Mahlatse Skudu Makudubela “Waziri wa Raha”, ametangaza rasmi kustaafu soka la kulipwa, akihitimisha safari ya miaka 17 iliyosheheni mafanikio, mataji na kumbukumbu nyingi ndani na nje ya bara la Afrika.
Nyota huyo wa Afrika Kusini amewahi kuzitumikia klabu kadhaa zenye heshima kubwa zikiwemo Mamelodi Sundowns, Orlando Pirates, Chippa United, Young Africans SC, AS Vita Club na Wiliete FC. Katika kipindi hicho alifanikiwa kutwaa mataji mbalimbali, yakiwemo MTN8, Telkom Cup pamoja na ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara (NBC Premier League) akiwa na Yanga SC.
Kupitia taarifa yake ya kuaga soka, Skudu amesema kuwa safari yake ilianza mwaka 2004 katika SAFA Transnet School of Excellence kabla ya kucheza soka la kulipwa katika nchi mbalimbali kama Afrika Kusini, Jamhuri ya Czech, Georgia, Tanzania, DR Congo na Angola. Ameeleza kuwa kila klabu aliyochezea na kila uwanja aliokanyaga vimemjenga kuwa mtu na mchezaji bora.
Aidha, ametoa shukrani kwa vilabu vyote alivyovitumikia, makocha, wachezaji wenzake, madaktari, wahudumu wa vifaa pamoja na mashabiki waliomuunga mkono katika kipindi chote cha maisha yake ya soka. Amesema mchezo huo umemfundisha nidhamu, umoja na upendo, huku ukimpa fursa ya kutimiza ndoto zake.
Skudu pia ameweka wazi kuwa hataachana na soka kabisa, kwani hatua yake inayofuata ni kuingia kwenye taaluma ya ukocha. Amesema sasa ni wakati wa “kutundika daruga” na kushika filimbi, akiwa na dhamira ya kuendelea kuchangia maendeleo ya mchezo kupitia benchi la ufundi. Wakati wa kuitumikia Yanga SC, Makudubela alikuwa mmoja wa viungo waliowavutia mashabiki kutokana na ubunifu wake, uwezo wa kutengeneza nafasi na staili yake ya kipekee uwanjani, hali iliyomfanya apewe jina la utani la “Waziri wa Raha.”
Kwa kustaafu kwake, soka linaaga mmoja wa viungo wenye kipaji kikubwa waliopita katika ligi mbalimbali barani Afrika. Tunamtakia kila la heri Mahlatse “Skudu” Makudubela katika safari yake mpya ya ukocha na maisha baada ya soka.