Kiungo mahiri wa Nigeria, Morice Chukwu, ameachana na mpango wa kuendelea kuitumikia Singida Black Stars baada ya kugomea mkataba mpya, huku akielezwa kuwa karibu kutua kwa mabingwa wa Tanzania Bara, Yanga SC.
Chukwu ambaye alikuwa sehemu muhimu ya kikosi cha Singida BS, hayupo kwenye timu hiyo inayojiandaa kushiriki michuano ya CECAFA Kagame Cup nchini Rwanda. Hatua hiyo imeongeza nguvu kwenye taarifa za kuondoka kwake baada ya kushindwa kufikia makubaliano mapya na waajiri wake.
Taarifa kutoka ndani ya uongozi wa Yanga zinaeleza kuwa klabu hiyo tayari imekamilisha hatua kubwa za kumsajili kiungo huyo mwenye uwezo wa kucheza nafasi zaidi ya moja uwanjani, ikiwemo kiungo wa kati na beki wa kati.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, ni suala la muda tu kabla Yanga haijamtambulisha Chukwu rasmi kama mchezaji mpya wa klabu hiyo na kuanza safari yake mpya akiwa na Wananchi ambao tayari wameanza maandalizi ya msimu ujao katika kambi ya Avic Town.
Chukwu anatarajiwa kuziba pengo la Mohamed Damaro ambaye Yanga ilikuwa na mpango wa kumsajili moja kwa moja baada ya kumalizika kwa mkataba wake wa mkopo wa miezi sita. Hata hivyo, mpango huo umefutwa na Damaro kurejea Singida BS ambako bado ana mkataba.
Usajili wa Chukwu unatarajiwa kuongeza nguvu kwenye kikosi cha Yanga kutokana na uwezo wake wa kucheza nafasi mbalimbali na uzoefu wake kwenye soka la Tanzania. Mabingwa hao wanaendelea kufanya maboresho ya kikosi chao wakielekea msimu mpya wenye changamoto ndani na mashindano ya kimataifa.