Simba SC imetangaza ujio wa Simba Marathon, tukio litakalokuwa sehemu ya mwendelezo wa shughuli za maadhimisho ya miaka 90 ya klabu hiyo. Tukio hilo linatarajiwa kufanyika Oktoba 4, 2026, likilenga kuwapa mashabiki nafasi ya kushiriki katika shughuli mbalimbali nje ya uwanja wa soka.
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba SC, Ahmed Ally, amesema maandalizi ya tukio hilo yanaendelea huku klabu ikilenga kuwaunganisha mashabiki kupitia shughuli zinazokwenda sambamba na utamaduni wa klabu hiyo.
Ahmed amesema Simba inaamini mashabiki wake wana vipaji na shughuli mbalimbali wanazozipenda nje ya mpira, hivyo Simba Marathon ni sehemu ya juhudi za kuwapa nafasi ya kushiriki, kufurahia na kuendelea kuwa karibu na klabu yao katika kipindi cha maadhimisho ya miaka 90.



