Rais wa Yanga SC, Mhandisi Hersi Said, amesema klabu hiyo inalenga kufanya vizuri katika Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu, ikiwemo kufika hatua ya fainali na kuwania ubingwa wa michuano hiyo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa tawi jipya la Yanga jijini Gaborone, Botswana, Hersi amesema Gaborone United ni timu nzuri, lakini Yanga imejiandaa vyema na haijaenda Botswana kwa ajili ya kushiriki tu. Amesisitiza kuwa endapo watafika fainali, dhamira yao ni kuhakikisha wanabeba kombe hilo.
Hersi pia ameeleza kuwa uzinduzi wa tawi hilo unalenga kuwapa wanachama wa Yanga wanaoishi nje ya Tanzania fursa ya kupata huduma na kutekeleza haki zao za uanachama. Amesema tawi hilo lina wanachama 63, idadi inayozidi mahitaji ya kikatiba ya wanachama 20 kwa ajili ya kuanzisha tawi.
Aidha, Rais huyo amesema tawi la Gaborone ni la 18 la Yanga lililoanzishwa nje ya Tanzania, akieleza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya ukuaji wa chapa ya klabu na mtandao wake wa wanachama na mashabiki katika mataifa mbalimbali.