Yanga SC imeanza kampeni yake ya kimataifa kwa kupata sare muhimu ya bao 1-1 ugenini dhidi ya Gaborone United, katika mchezo wa mkondo wa kwanza wa hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Yanga ilionyesha kiwango kizuri kwa kutawala mchezo kwa muda mwingi, lakini ilikumbana na ukuta mgumu wa Gaborone United ambao walitumia muda mwingi wa mchezo wakijilinda kwa wachezaji wengi.
Gaborone United ndio waliokuwa wa kwanza kupata bao dakika ya 33 kupitia mpira wa adhabu uliopigwa nje kidogo ya eneo la 18. Obry Amseb aliucheza kwa ustadi mpira huo na kuipatia timu yake uongozi wa 1-0.
Baada ya bao hilo, Yanga iliendelea kulisakama lango la wenyeji, huku Gaborone United wakionekana kuridhika zaidi na kujilinda ili kuhifadhi uongozi wao.
Hata hivyo, wakati mchezo ukielekea dakika za mwisho na wenyeji wakiamini wangeondoka na ushindi, Seleman Mwalimu 'Gomez' alivuruga sherehe hiyo kwa kufunga bao la kusawazisha dakika za lala salama.
Bao hilo lilianza na pasi ya Maxi Nzengeli iliyopenya kwenye safu ya ulinzi ya Gaborone United na kumfikia Mudathir Yahya. Mudathir hakusita, akatoa pasi ya kisigino iliyomkuta Mwalimu, ambaye alimalizia kwa ustadi na kuifanya Yanga isawazishe 1-1.
Kwa ujumla, dakika zote 90 zilitawaliwa zaidi na Yanga, huku changamoto kubwa ikiwa ni namna ya kuvunja ukuta wa Gaborone United ambao walijilinda kwa wachezaji wengi.
Sare hiyo ni matokeo muhimu kwa Yanga, ambayo sasa itakuwa na dakika 90 za nyumbani kusaka ushindi utakaoiwezesha kufuzu hatua inayofuata. Timu hiyo pia itaingia kwenye mchezo wa marudiano ikiwa na faida ya bao ililofunga ugenini.