Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo chini ya Waziri Paul Makonda imepanga kuunda kamati maalumu ya kuchunguza mkataba wa mzabuni wa jezi za timu za taifa, huku ikitaka kubaini manufaa ya mkataba huo kwa timu zinazowakilisha Tanzania.
Hatua hiyo imekuja baada ya kuzuka sintofahamu kuhusu jezi mpya za Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, huku Wizara ikitaka kupata ufafanuzi kuhusu mkataba huo na namna unavyowanufaisha timu za taifa ambazo zimekuwa zikigharamiwa na Serikali.
Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara, uchunguzi huo utalenga kupitia mkataba huo na kubaini iwapo masharti yake yanaendana na maslahi ya timu za taifa pamoja na uwekezaji unaofanywa na Serikali katika kuzigharamia timu hizo.
Wizara pia imeweka wazi kuwa suala hilo linahitaji kufanyiwa uchunguzi ili kupata uelewa wa kina kuhusu mkataba wa mzabuni huyo na manufaa yanayopatikana kwa upande wa timu za taifa.