Klabu ya CFFA ya Madagascar inatajwa kuomba kutumia Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam, kwa ajili ya mchezo wake wa nyumbani dhidi ya Yanga SC katika hatua ya kuwania kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika (CAFCL).
Hatua hiyo inaweza kuifanya Yanga kucheza michezo yote miwili ya hatua hiyo nchini Tanzania, jambo linaloweza kuwa na umuhimu mkubwa kwa Wananchi katika harakati zao za kutafuta nafasi ya kufuzu hatua ya makundi ya michuano hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa, CFFA imelazimika kutafuta uwanja mbadala baada ya kukosekana kwa uwanja nchini Madagascar uliopitishwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kwa ajili ya kutumika katika michuano hiyo.
Inaelezwa kuwa klabu hiyo tayari imewasilisha Uwanja wa Azam Complex kwa CAF kama uwanja wake wa nyumbani kwa ajili ya mchezo wa kwanza dhidi ya Yanga.
Yanga kupata nafasi ya kucheza mechi zote nyumbani
Kwa mujibu wa ratiba, mchezo wa kwanza kati ya CFFA na Yanga unatarajiwa kuchezwa Oktoba 17, huku mchezo wa marudiano ukipangwa kufanyika Oktoba 24 katika Uwanja wa Azam Complex.
Iwapo ombi la CFFA litakubaliwa na CAF, Yanga itakuwa na nafasi ya kucheza michezo yote miwili katika uwanja huo, ambao pia inautumia katika kampeni zake za kimataifa.
Hali hiyo inaweza kuwa na manufaa kwa Yanga kwa kupunguza changamoto za safari za kimataifa na kuipa timu mazingira inayoyafahamu katika michezo yote miwili.Β