Kocha wa Young Africans (Yanga), Simon Dladla, amewataka mashabiki wa klabu hiyo kujitokeza kwa wingi uwanjani apo kesho katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, akieleza kuwa sapoti yao ni muhimu katika kuwapa wachezaji hamasa ya kupambana na kutafuta ushindi.
Akizungumza na waandishi wa habari kuelekea mchezo huo, Dladla amesema uwepo wa mashabiki ni sehemu muhimu ya nguvu ya timu, hasa katika kipindi hiki ambacho Yanga inaendelea kupambana kutimiza malengo yake ya msimu. huku akisisitiza kuwa sapoti ya Wananchi inaweza kuongeza morali na kuifanya timu kuwa na msukumo zaidi ndani ya uwanja.
Kocha huyo pia ameeleza kuwa benchi la ufundi linaendelea kufanya kazi kila siku kuboresha kikosi na kurekebisha mapungufu yanayojitokeza katika michezo mbalimbali. Hata hivyo, amesema juhudi hizo zinahitaji kuungwa mkono na mashabiki ambao wamekuwa sehemu muhimu ya safari ya klabu hiyo.
“Tunahitaji sana nguvu na hamasa kutoka kwa Wananchi, kwani uwepo wenu uwanjani huwapa wachezaji morali na motisha ya kupambana kwa ajili ya ushindi,” alisisitiza Dladla.
Wito huo unakuja wakati Yanga ikiendelea na kampeni yake ya kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Bara. Dladla anatarajia kuona mshikamano kati ya timu na mashabiki ukiendelea kuimarika, huku Wananchi wakitakiwa kujitokeza kwa wingi na kuwa sehemu ya nguvu itakayoisukuma timu kuelekea malengo yake ya msimu.