Nahodha wa Yanga SC, Bakari Mwamnyeto, amefafanua uhusiano wake na mlinda lango Djigui Diarra, akisema kuwa licha ya wakati mwingine kugongana uwanjani, wawili hao wana mawasiliano mazuri ndani na nje ya uwanja.
Mwamnyeto amesema Diarra ni miongoni mwa wachezaji ambao amekuwa akiwasiliana nao mara kwa mara, akieleza kuwa mawasiliano yao hayahusiani na masuala ya uwanjani pekee, bali pia hupigiana simu na kujadili mambo mbalimbali yanayohusu timu.
Mwamnyeto amesema tofauti au kugongana kunakoweza kuonekana wakati wa mchezo si ishara ya uhasama kati yao, bali ni sehemu ya mawasiliano na majukumu yao ndani ya timu.
Msimu uliopita baada ya mchezo wa ligi kuu dhidi ya Dodoma Jiji ambao Yanga walifungwa mabao 3-2 yalizungumzwa mengi kufuatia Diarra kuomba kutoka baada ya bao la kujifunga la Mwamnyeto.
Hata hivyo Yanga ilitoa ufafanuzi kuwa Diarra alipata majeraha na kulazimika kutoka nafasi yake ikichukuliwa na Hussein Masalanga.
Lakini wengi walitafsiri kuwa aliomba kutoka baada ya kupishana kauli na Mwamnyeto ambaye hatimaye naye amefafanua ukweli wa sakata hilo.
Wawili hao wameendelea kuwa nguzo muhimu ya safu ya ulinzi ya Yanga katika misimu minne ambayo wamecheza pamoja ndani ya kikosi cha Yanga.