Baada ya kukosa mchezo wa ligi kuu dhidi ya Simba akitumikia adhabu ya kadi nyekundu, kiungo mshambuliaji wa Yanga Stephane Aziz Ki anatarajiwa kurejea kikosini mwishoni mwa wiki wakati Yanga itakapomenyana na CFFA ya Madagascar kwenye mchezo wa kwanza kuwania tiketi ya kutinga hatua ya makundi ligi ya Mabingwa (CAFCL)
Kurejea kwa Aziz Ki ni habari njema kwa kocha Manqoba Mngqithi kwani anatarajiwa kuongeza ubunifu katika safu ya ushambuliaji.
Yanga inahitaji kushinda mchezo huo utakaopigwa uwanja wa Azam Complex ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kufuzu hatua ya makundi pale timu hizo zitakaporudiana siku nne baadae kwenye uwanja huohuo.
CFFA iliwasili nchini jana ambapo leo kikosi hicho kimeanza maandalizi tayari kuwakabili mabingwa hao wa Tanzania Bara.
Upande wa Yanga, kikosi kiliingia kambini baada ya mchezo dhidi ya TRA United kusogezwa mbele, Wananchi wakipata muda wa kutosha kujiandaa na mchezo wa ligi ya mabingwa.
Hata hivyo wakati Aziz Ki akirejea, Yanga imepata pigo wakitarajiwa kumkosa kiungo kiraka Duke Abuya aliyeumia kwenye mchezo dhidi ya Simba.
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga Ali Kamwe alisema Abuya anaweza kukosekana kwa kipindi cha wiki mbili hadi tatu.