Kikosi cha Yanga leo majira ya saa 1 usiku kitashuka uwanja wa Azam Complex, Chamazi kuhitimisha mchezo wa mkondo wa pili kuwania tiketi ya kutinga hatua ya makundi ya ligi ya mabingwa dhidi ya CFFA ya Madagascar.
Wananchi leo wako nyumbani baada ya mchezo wa kwanza ugenini ambao waliandikisha ushindi wa mabao 4-0 hapohapo Azam Complex.
Ni wazi CFFA leo watahitaji muujiza kuweza kuiondosha Yanga kwani kimahesabu watahitaji kushinda angalau mabao 5-0 ili kufuzu moja kwa moja.
Kwa upande wa Yanga hali ni tofauti, kikosi cha kocha Manqoba Mngqithi kitaingia kwenye mchezo huo bila ya kuwa na presha kubwa kwani zaidi ya nusu ya kazi wameshaimaliza.
Hata hivyo Manqoba amesema wataingia dimbani bila ya kujali kile walichovuna kwenye mchezo wa kwanza wakihitaji kupata ushindi.
Kumekuwa na ukosoaji wa hapa na pale baada ya mchezo uliopita hivyo leo wachezaji wa Yanga wanatarajiwa kushuka Azam Complex wakifahamu wana deni kubwa kwa mashabiki wao ambao wanataka wafanye zaidi ya kile walichofanya kwenye mchezo wa kwanza.
Eneo la safu ya ushambuliaji lilishushiwa lawama nyingi kutokana na kupoteza nafasi za wazi, leo ni siku ya kudhihirisha kile walichofanyia kazi kwenye uwanja wa mazoezi.
Ushindi kwa Yanga leo utawahakikishia kufuzu hatua ya makundi ya CAFCL kwa msimu wa nne mfululizo na kuweka rekodi ya kuwa timu ya kwanza Tanzania kufikia mafanikio hayo.